CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewaondoa masomoni wanafunzi 121 waliopatikana na hatia ya kuhusika kuchezea matokeo ya mitihani.
Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha chuo hicho imeeleza kuwa wanafunzi 170 walituhumiwa kuchezea Mfumo wa matokeo (SR2) 2023/2024.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali iliunda kikosikazi kilichohusisha wataalamu wa mifumo ya komputa kuchunguza tuhuma hizo na iliwasilisha ripoti yao Udom.
Ilieleza kuwa baada ya kupokea ripoti hiyo, hatua za ndani zilianza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwaita watuhumiwa waende kusikilizwa kabla ya kutoa uamuzi kwa mujibu wa kanuni zilizopo.
“Jumla ya wanafunzi 148 walisikilizwa, wanafunzi 32 hawakufika kusikilizwa. Katika wanafunzi waliosikilizwa, wanafunzi 121 walipatikana na hatia ya kuhusika kuchezea matokeo ya mitihani na kikao cha Seneti ya Chuo kupitisha kuondolewa masomoni,” ilieleza taarifa hiyo.
Iliongeza: “Kesi za wanafunzi 15 zinaendelea na uchunguzi zaidi. Wanafunzi wawili hawakukutwa na hatia.”
Taarifa ilieleza kwamba kwa mujibu wa taratibu za Udom, mwanafunzi ambaye hajaridhika na uamuzi wa seneti anapewa nafasi ya kukata rufaa.
“Hivyo wanafunzi ambao hawajaridhika, taratibu ziko wazi, wana fursa ya kukata rufaa kupitia mifumo iliyowekwa na chuo,” ilieleza.
Iliongeza: “Dirisha la rufaa hufunguliwa wiki mbili baada ya matokeo ya mitihani kutokana na kufungwa baada ya wiki mbili. Mwanafunzi ambaye yupo nje ya muda, anaruhusiwa wakati wowote kuomba kukata rufaa nje ya muda. Chuo kitaendelea kusimamia taratibu, kanuni na sheria za kimitihani ili kulinda ubora wa taaluma na hadhi ya chuo, pasipo kumuonea yeyote.
0 Comments