HABARI

6/recent/ticker-posts

WANANDOA WAELEZA WALIVYOANZISHA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA.

 


WASHITAKIWA Minda Mussa na mkewe Fatuma Kassim wanaokabiliwa na kesi ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu namna walivyoanza kujihusisha na biashara hiyo.

Washitakiwa walidai hayo kwa njia ya maelezo waliyoandika wenyewe na kusomwa na Wakili wa Serikali, Aron Titus mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo wakati kesi hiyo ilipoletwa mahakamani hapo kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya makosa yao na ushahidi utakaotumika katika kesi hiyo.

Minda alidai yeye na familia yake walianza kujihusisha na biashara hiyo baada ya yeye (Minda) kuacha kazi ya ulinzi aliyokuwa anafanya na kukutana na rafiki yake anayeitwa Kizota aliyekuwa akiishi katika eneo la Kimboka, Buguruni Dar es Salaam.

“Rafiki yangu Kizota aliyekuwa anaishi Kimboka Buguruni, ndiye aliyenishawishi kuingia kwenye biashara hii wakati nikiwa nimetoka kuacha kazi zangu za ulinzi,” alidai Minda.

Kwa upande wake, Fatuma alidai kuwa aliacha biashara hiyo tangu walipokamatwa mara ya kwanza mwaka 2011 na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja.

“Tangu wakati ule nilipotoka jela sikuwahi tena kujihusisha na biashara hii, hata mume wangu nilishamsihi tuache kwa usalama wetu ila hakunisikia akaendelea,” alidai Fatuma kupitia maelezo yake.

Aidha, upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kesi hiyo itaanza kusikilizwa katika Mahakama kuu divisheni ya Uhujumu Uchumi.

Wakili Titus alidai kuwa watakuwa na mashahidi 11, vielelezo vya maandishi saba na vielelezo vya kushikika sita.

Hati ya mashitaka ilidai washitakiwa wote kwa pamoja wanashitakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa gramu 375.20 na upelelezi umekamilika na wapo kwenye taratibu za kupeleka jalada mahakama kuu divisheni ya uhujumu uchumi.

Ilidaiwa kuwa Novemba 23, 2017 eneo la Chamazi Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa gramu 375.20.

Post a Comment

0 Comments