DAR ES SALAAM: TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kesho inaanza awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura kwa ajili ya kutoa fursa kwa wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa zao na kuweka pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa.
Taarifa iliyotolewa na INEC Aprili 14, 2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele inaeleza kuwa uboreshaji huo utafanyika kwa mizunguko mitatu huku mzunguko wa kwanza ukijumuisha mikoa 15, mzunguko wa pili mikoa 16 na mzunguko wa tatu utajumuisha vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo.
Baada ya taarifa hiyo kutolewa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umetoa wito kwa vijana nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika awamu hiyo ili kutimiza haki yao kikatiba
Wito huo ulitolewa Dar es salaam jana Aprili 29,2025 na Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi Taifa,Jessica Mshama wakati akizungumza na Waandishi wa Habari.
Alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na INEC awamu hiyo itakuwa na jumla ya vituo 7,869 vitakavyotumika Tanzania Bara vituo 7,659 na Zanzibar vituo 210.
“Uboreshaji huu utakwenda kwa awamu tatu,awamu ya kwanza itaanza Mei mosi hadi 7 na itakuwa na mikoa 15 ambayo ni Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe,awamu ya pili ni Mei 16 hadi 22 katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba,”alieleza taarifa hiyo
Iliongeza,”mzunguko wa tatu utaanza 28 Juni – 04 Julai na utahusisha vituo vya magereza 130 Tanzania Bara na vyuo vya mafunzo 10 Zanzibar na tunatarajia kuwa katika awamu hii ya uboreshaji, wapiga kura wapya 1,396,609 wataandikishwa, wapiga kura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 148,624 watafutwa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari,”
Pia, Mshama amewaonya UVCCM kutoshirikiana na viongozi wenye nia ovu ya kutaka kuleta uvunjifu wa amani na kusisitiza kuwa Tanzania inaongozwa kwa misingi ya sheria na Katiba kwasababu kila kijana ana haki ya kushiriki kwa uhuru na amani katika mchakato wa uchaguzi hivyo wasidanganyike na watu wasiokuwa wazalendo kwa taifa.
Mshama alieleza kuwa katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, vijana wana kila sababu ya kujivunia uongozi wake kwasababu ametengeneza zaidi ya ajira milioni nane kupitia sekta za umma na binafsi kwa muda mfupi ambayo ni sawa na asilimia 115 pamoja na fursa za ajira katika sekta za elimu na afya.
Amesema Rais Samia amefanikisha ukamilishaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ni Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Reli ya Kisasa ya SGR,Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.
Amebainisha kuwa zaidi ya Sh bilioni 250 zimetolewa kwa makundi ya vijana kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo kiuchumi na kujitegemea.
kusisitiza vijana kujiandikisha, kuboresha taarifa zao, kuchangamkia fursa za kugombea nafasi za uongozi, na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi unaokuja. Tanzania ya sasa inahitaji viongozi vijana wenye maono, uadilifu na uzalendo wa dhati
Amesema ni wakati wa UVCCM kusimama na kueleza mafanikio makubwa yaliyofanikishwa na serikali ikiwa ni pamoja huduma ya maji safi kwa vijijini 9,259 kati ya 12,318 sawa na asilimia 75.
Kwa sasa upatikanaji wa maji umefikia asilimia 77 vijijini na 88 mijini hivyo kuondoa adha ya upatikanaji wa maji, ujenzi wa shule mpya 3,631 za msingi na sekondari na madarasa 21,912 yameongezwa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi
Amesema serikali ya awamu ya sita imejenga vituo vya afya 367 na Zahanati 980 ili kuimarisha huduma za afya na kupunguza vifo vya wajawazito ambavyo vimepungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000.
Aidha amesema Bima ya Afya imeimarishwa ili wananchi wapate matibabu kuanzia Zahanati hadi Hospitali za Rufaa pamoja na kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo yamefikia asilimia 85.
0 Comments