HABARI

6/recent/ticker-posts

SAMIA KUIFUNGUWA TANGA NA PEMBA KIUCHUMI.



 TANGA; RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanga inakwenda kufunguka kiuchumi kwani serikali inapanga kuunganisha Tanga, Unguja na Pemba kwa usafiri wa maji kutokana na Kisiwa cha Pemba kwa kiasi kikubwa kutumia mazao ya kilimo kutoka Tanga.

Katika siku ya pili ya ziara yake ya siku saba mkoani Tanga, Rais Samia alisema kwa tathmini yake ya juzi na jana, ameona kuwa fedha zinazotolewa na serikali kuondoa shida za wananchi kweli zimeondoa shida hizo na fedha zimetumika.

Akizungumzia jengo la Halmashauri ya Bumbuli alilozindua, aliwataka watumishi watakaokuwa wakilitumia kulitunza na kutoa huduma nzuri kwa wananchi

Aidha DKT Samia Suluhu Hassan Akiagiza ;Watu wa Halmashauri ya Bumbuli, hongereni jengo ni zuri litumieni kwa huduma mnazozitaka pia litunzeni na wafanyakazi wa mule ndani jengo ni zuri kwa nje, lifanyeni liwe zuri pia ndani kwa huduma za nzuri kwa wananchi

Alisema katika kipindi chake cha uongozi, halmashauri 122 kote nchini zimepata majengo mapya ya namna hiyo.

Aliwapongeza wananchi wa Lushoto kwa kuwa watunzaji wazuri wa mazingira na kwamba hata uvutaji wa hewa Lushoto ni mrahisi kutokana na mazingira mazuri na kuwataka wawafundishe wengine ili waige mfano wao.

 

Pia, alisema kumekuwa na changamoto ya wanyama waharibifu wanaoingia kwenye mashamba ya watu na kuwa serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuwalinda wananchi ikiwamo kuongeza askari wa wanyamapori na kubuni mbinu mbalimbali za kufukuza wanyama ikiwamo matumizi ya ndege nyuki.

“Nataka nimwagize Waziri wa Utalii aone uwezekano wa kufanya mapitio ya kanuni za kulipa fidia, wale ambao wanaingiliwa na wanyama kwenye mashamba yao wakaangalie kuhakikisha kwamba kweli fidia inayotoka inamlipa mwananchi jasho lake baada ya kuharibiwa na wanyama

Alisema Machi 6, mwaka huu itafunguliwa zabuni ya kutafuta mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Soni – Bumbuli – Korogwe yenye kilometa 77.

Nae Raisi alisema ;Barabara hii mwanangu January (Mbunge wa Bumbuli, January Makamba) amekuwa akiililia na baada ya kusikia kilio chake nikasema tangazeni zabuni, tunakwenda kujenga kilometa 22 kuanzia Soni kwenda Bumbuli na kilometa 9.3 tutajenga kutoka Kwameta hadi Kwashemsi

Aliongeza: “Kwa Tanga pia tumekwenda kujenga barabara ya Bagamoyo – Pangani – Tanga na keshokutwa nikiwa Pangani nitakwenda kuweka jiwe la msingi kuzindua Daraja la Pangani”.

Aidha, alisema ununuzi wa chai bado unasuasua pamoja na viwanda viwili vilivyokuwa vimefungwa kufunguliwa na kuwa serikali inaweka mambo sawa na itanunua chai yote inayozalishwa Lushoto pamoja na kuvutia wawekezaji wa uhakika ili chai yote ya wakulima ipate soko.

“Waziri wa Kilimo ana mpango mzuri sana kuhusu zao la chai kwa hiyo wakulima wa chai nataka niwape moyo kwamba tunalielewa tatizo lenu na tunalifanyia kazi,” alibainisha Rais Samia.

Kwa upande wa maji, alisema Lushoto kazi haijafanyika vizuri sana lakini kuna miradi mingi ya maji ambayo kabla ya muda wa kupiga kura mengine itakuwa imekamilika.

“Mradi wa Mkomazi umezungumzwa miaka mingi lakini haujafanyiwa kazi, awamu hii tumeamua kuufanyia kazi tunakwenda kuweka bwawa kubwa litakaloweka maji mengi yatakayowafaa wakulima na wanyama na matumizi mengine,” alieleza.

Mbunge wa Bumbuli, January alimshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumteua katika nafasi za uwaziri ambazo alishawahi kuzitumikia na kuwa ni heshima kubwa ambayo haitafutika katika maisha yake.

“Katika kipindi ambacho nimefanya kazi na wewe nimejifunza sana na nimeerevuka sana kutokana na uongozi wako na kabla ya hapo nilikuwa Waziri wa Nchi chini ya ofisi yako tumefanya kazi miaka minne na ilikuwa ndio nafasi yangu ya kwanza ya uwaziri, wewe ndio umenifundisha mimi kuwa waziri kwa hiyo kama kuna werevu nilionao kwenye uwaziri, basi umetokana na mkono wako,” alieleza.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema amemsamehe January.

Alisema alikuwa amempiga kofi January kama adhabu ya mama kwa mtoto na sasa amemrudisha kwa mama.

“Nataka nimwite mwanangu Januari hapa aje arudi kwa mama, sisi wamama mnatujua ukimkera mama anakupiga kakofi anakufichia chakula, sasa mwanangu nilimpiga kofi nikamfichia chakula, lakini leo namrudisha kwa mama,” alisema Rais Samia.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alisema watayalinda mafanikio na mambo yote anayoyafanya Rais Samia kwa gharama na wivu.

“Wapotoshaji hawana nafasi, wenye fitna hawana nafasi, walaghai hawana nafasi, wakisema uongo tutasema ukweli hadharani,” alisema Makala

Post a Comment

0 Comments