Kenya inakabiliwa na mlipuko hatari wa ugonjwa wa Kalazar, ambapo watu 33 wamefariki na zaidi ya visa 1,000 vimeripotiwa katika muda mfupi. Hali hii imeibua maswali namna Afrika inavyoshughulikia magonjwa yaliyopuuzwa.
Kenya inakabiliwa na mlipuko hatari wa ugonjwa wa Kalazar, ambapo watu 33 wamefariki na zaidi ya visa 1,000 vimeripotiwa katika kipindi cha miezi minne pekee. Hali hii imeibua wasiwasi kuhusu namna bara la Afrika linavyoshughulikia magonjwa yaliyopuuzwa, hasa maeneo yenye huduma haba za afya.
Kalazar, au visceral leishmaniasis, ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya Leishmania, wanaoenezwa na mbu wadogo. Ukiachwa bila kutibiwa, ugonjwa huu unaweza kusababisha vifo kwa zaidi ya 95% ya waathirika. Visa vingi vimeripotiwa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya, yakiwemo kaunti za Wajir, Garissa, na Marsabit.
Mary Muthoni, Katibu Mkuu katika Wizara ya Afya, amesema kuwa maambukizi yamefikia 1,041 hadi sasa: "Tayari tuna vifo 33, na hii inasikitisha sana," alisema.
Wizara ya Afya imetuma maabara tatu za rununu na dawa katika maeneo yaliyoathirika, huku wahudumu wa afya wakishirikiana na serikali za kaunti
"Tumeweza kuimarisha ufuatiliaji wetu... na kupeleka vifaa muhimu vya tiba," alisema Muthoni.
Kaunti ya Wajir ndiyo iliyoathirika zaidi. Gavana Ahmed Abdulahi ameeleza kuwa wameongeza uwezo wa hospitali, kupanua wodi za wagonjwa, na kuanzisha ufukizaji wa makaazi vijijini.
"Sasa wagonjwa wengi wanaondoka hospitalini baada ya kupata nafuu," alisema Gavana Abdulahi.
Hata hivyo, licha ya Kenya kutangaza Kalazar kama janga, ugonjwa huu bado haupewi uzito unaostahili ikilinganishwa na magonjwa mengine. Wataalamu wanahoji kuwa hali hii ni mfano wa changamoto pana zaidi barani Afrika kuhusu magonjwa yaliyo katika kivuli cha utafiti na uwekezaji.
Kwa mujibu wa Dkt. Daniel Masiga kutoka ICIPE, eneo la Afrika Mashariki lilichangia 73% ya visa vya Kalazar duniani mwaka 2022, nusu yao wakiwa watoto chini ya miaka 15. Kenya, Ethiopia, Sudan na Brazil zilichangia kwa pamoja 60% ya visa vyote duniani.
Dkt. Masiga anasema kuna matumaini kupitia utafiti, maendeleo ya chanjo, na utengenezaji wa dawa mpya.
"Hii ni fursa ya kukomesha magonjwa haya yaliyopuuzwa," anasisitiza.Kwa sasa, jibu la haraka na la pamoja linahitajika, si tu kwa Kenya bali kwa Afrika nzima, ili kuhakikisha kuwa magonjwa yaliyopuuzwa hayasababishi maafa ya kimya kimya.
0 Comments